TAMKO LA POLISI KUHUSU ZOEZI LA KUAPISHWA SERIKALI ZA MITAA
Kufuatia
kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa,
Vijiji na Vitongoji na hivi sasa kuendelea kwa zoezi la kuapishwa kwa
viongozi hao katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kumejitokeza tabia ya
baadhi ya wananchi kufanya vurugu na fujo katika zoezi hilo.Baadhi
ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kufanya
fujo na vitendo vya vurugu ikiwemo kuwapiga baadhi ya watendaji
wanaosimamia zoezi la kuapisha na kuwapiga viongozi wateule
waliochaguliwa kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda kihalali
katika uchaguzi huo jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na
taratibu za nchi.Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kwa wananchi wenye tabia hiyo kuacha
mara moja na badala yake kama mtu hakuridhika na matokeo ya uchaguzi
huo, afuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye ngazi husika
ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.Aidha,
Jeshi la Polisi linawata Wakurugenzi na Maafisa watendaji wenye dhamana
ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti waliochaguliwa,
kufuatilia kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua migogoro hiyo
mapema ili kuepusha migongano inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Jeshi
la Polisi halitamvumilia mtu ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu
ama fujo kwa kisingizio cha ushabiki wa siasa na badala yake
atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Advera J. Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
0 comments: