USILIE, MAPENZI NI MATAMU LAKINI SIYO RAHISI.. BOFYA HAPA
Kwa nini mapenzi ni tata?
Unaweza kujiuliza swali hilo. Ni kwa faida ya kila mmoja kwa sababu
yanatuhusu sote. Ni matamu lakini ndani yake hutokea kuwa na ukakasi
kama siyo maumivu.
Jiulize
tena, kwa nini mapenzi yanasumbua? Mapenzi ni maumivu ya kichwa na
moyo. Watu wengi waliomo ndani yake wanaweza kukupa ushuhuda wa mateso
wanayoyapata kwenye uhusiano wao. Je, baada ya kuteseka huwa wanajiapiza
kutorudi tena?
La
hasha! Wanajaribu mara nyingi, hawakomi. Unaweza kujiuliza ni kwa nini
lakini ukweli ni kwamba pamoja na maumivu ambayo mtu anaweza kuyapata
kwenye mapenzi, bado yanabeba hisia kubwa katika maisha ya kila
binadamu.
Maisha
bila mapenzi hayajakamilika. Kutokana na hilo, uwanja upo wazi kwako
kujiuliza ni kwa nini kitu kitamu namna hiyo kikafanywa kuwa tata,
jumlisha na maumivu ya hapa na pale. Uvumilivu ukizingatiwa, huyeyusha
utata unaojitokeza mara kwa mara.
Muhimu
zaidi ni kwamba mapenzi hayatoshelezi kwa uwajibikaji wa nusu nusu.
Yanahitaji nidhamu na utekelezaji wa moja kwa moja kutoka moyoni.
Yanayomhusu mwenzi wako ni vyema uyabebe kama yako, hivyo ndivyo
uhusiano unavyotaka.
Mapenzi
yanahitaji akili, utashi na fikra zako bila kusahau nguvu zote katika
kuzalisha matunda ya kila siku kwenye uhusiano ulionao. Utata
unaoonekana ni ule unaotokana na wenzi kutotimiza matarajio ya kila
mmoja.
Imetokea
kuamini kuwa maneno ni mhimili wa kudumu kwa uhusiano na kukutana
kimwili husuluhisha migogoro ya muda mfupi. Wapenzi wanaponuniana,
endapo watakutana faragha, hasira zote hupotea. Hata hivyo, kwa bahati
mbaya, ni zaidi ya kutosheka kimwili na utamu wa maneno mazuri.
Kwa
mfano, ndoa nyingi zinakumbwa na matatizo ya watu kushindwa kuwa
wakweli. Mwanaume au mwanamke anaweza kusema ni kiasi gani mwenzi wake
anamuumiza. Lakini mwisho wa mazungumzo hawezi kukiri kasoro zake ambazo
pengine ndiyo chanzo cha kila kitu.
Utata
zaidi katika mapenzi ni kuwa, inapotokea watu wanajuana kwa undani mno,
hasa baada ya kuishi muda mrefu, ni hapo ndipo maneno hayawezi kufaa
kitu, wala mchezo wa faragha hautaleta maelewano kwa maana hakuna kitu
kigeni.
Lingine
la utata katika mapenzi ni kwamba huwezi kuficha tabia yako muda wote.
Ukishazoeana na mwenzi wako hasa baada ya kuwa pamoja muda mrefu,
utaanza kujiachia. Ni kipindi ambacho mmoja anaweza kuhisi amesalitiwa
kwa sababu mwanzoni hakuona hivyo ‘vitabia vya kuudhi’, alifichwa.
MAPENZI NI KARATA TATU
Kuna
msemo kuwa mapenzi hayashindwi ila watu ndiyo hushindwa na mapenzi.
Tunarukia kwenye uhusiano bila kuwa na uhakika ni kiasi gani tunawapenda
wenzetu na ni kwa kiwango kipi tumejiandaa kubeba majukumu.
Mwisho
wake tunafeli. Tatizo ni kwamba tunaanzisha uhusiano mpya bila kutatua
kasoro zilizosababisha tukashindwa kwenye uhusiano na mtu wa kwanza.
Hapo nadhani unaweza kuona kwamba wakati mwingine mapenzi siyo tata ila
wenyewe tunayafanya kuwa magumu.
Tuna
mambo mengi, ya kifamilia, kikazi, imani, dini, kabila, tofauti za
kimtazamo na matarajio ya kila mmoja. Hatuko sawa. Tunapoingia kwenye
uhusiano, fikra zetu zinakuwa zimejaa. Ajabu ni kwamba tunapoingia
kwenye uhusiano hatuyapi kipaumbele katika kuyajadili na kukubaliana.
Hisia za juu hutupeleka kama vipofu.
Uhusiano
wa kimapenzi wa watu wengi huanza pale ambapo mtu anajihisi yupo mpweke
na anahitaji kampani. Wakati mwingine inatokea kwa sababu mtu anakuwa
anakabiliwa na ‘presha’ ya kuwa na mwenzake kwa kigezo kwamba umri
umekwenda. Si kwamba amemuona mtu mwenye sifa anazohitaji.
Umri
ni kigezo kimoja lakini inawezekana ikawa mtu anataka kuwa na mwenzake
kwa sababu ya msukumo wa nafasi yake kwenye jamii au kimila. Pengine ni
dada sasa wadogo zake wameolewa yeye bado yupo tu. Au ni kaka, kwa hiyo
kama kiongozi wa familia anaona bora aoe mapema kabla ya wadogo zake.
Kama
umeingia kwenye uhusiano kwa sababu ya presha ya aina hiyo, utawezaje
kuwa na matunda sahihi? Kichocheo cha uhusiano wa kimapenzi kinapaswa
kuwa mapenzi. Mnapendana, kwa hiyo nyoyo zenu zinavutana kuingia kwenye
sayari maalum.
Usiwe
na papara, angalia mahitaji ya moyo wako, weka mbele matarajio yako.
Fikra zako uziweke wazi. Unapotafuta mwenzi hakikisha husumbuliwi na
presha yoyote. Jambo ambalo unapaswa kuamini ni kwamba aliye ndani ya
mawazo yako utampata kama ukijipa nafasi.
Kuna mambo ya kufanyia kazi, tukutane wiki ijayo ili tuendelee kujifunza kuhusu utata uliopo kwenye mapenzi.
0 comments: