BARUA NZITO: WOLPER JIHESHIMU BWANA
Kwako
mtoto mzuri unayekimbiza kwenye anga la filamu Bongo, Jacqueline Massawe Wolper. Bila shaka ni mzima wa afya na unaendelea na majukumu yako ya kila siku.
Binafsi mimi naendelea vizuri mambo yanakwenda kwenye mstari na leo nimekukumbuka kupitia barua nzito.
Nataka kusema na wewe mawili matatu ambayo mimi nimeona si sawa kufanywa na wewe!
Nisichelewe sana wala nini, madhumuni ya barua hii kwanza kabisa ni kutaka kukukumbusha kwamba unapaswa kujiheshimu katika kila sekta kwa kuwa wewe ni kioo cha jamii.
Jamii inakuheshimu, inakufuatilia kila hatua unayopiga maishani.
Wanaokufuatilia ujue wanakupenda ingawa pia hata wale wasiokupenda nao pia wanakufuatilia.
Wanakufuatilia kwenye vyombo vya habari, katika mitandao ya kijamii na hata live mitaani. Kauli yako lazima iwe na staha.
Sababu ya kukwambia jiheshimu ni kauli zako kwenye mitandao ya kijamii. Mara kadhaa nimekuwa nikiona ukiposti lugha ya matusi kwa waliokuudhi.Kwa nini utukane? Kwa mtu anayejiheshimu kama wewe si busara hata kidogo kutukana hata kama umechokozwa.
Akili yako inapaswa kutafakari kwa kina kabla ya kuposti kitu chochote katika mitandao ya kijamii. Unapoposti kitu pia ujue kuna watu ambao watakipenda na ambao hawatakipenda, sasa kwanza kuwajibu wale wasiokipenda unajishushia heshima!
Mfano mzuri ni siku ile ulipoweka aina mpya ya simu katika mtandao wa kijamii. Niliufuatilia mjadala ule, kuna watu walikuponda kwamba aina ya simu hiyo mpya haipo na kwamba ulifanya hivyo ili kujipa sifa.
Mtoto wa kike ukaona bora umtukane, ukaandika tusi zito kabisa kumjibu shabiki huyo. Ukimjibu mjinga unategemea nini? Najua kabisa dhamira yako kuweka simu hiyo ilikuwa ni utani lakini walivyoipokea baadhi ya mashabiki wakakusababisha utukane.
Wewe unaheshimika, kutukana si jambo la busara. Siku hizi teknolojia inakua, ni rahisi mtu kukufuatilia na kukupata na hata kukuchukulia hatua za kisheria.
Kwa nini utukane? Kwanza hata ukiamua kutukana, utatukana wangapi katika mitandao ya kijamii? Si sawa!
Siku hizi mitandao inatumika kama chombo cha biashara, ni vyema ukawa makini na unavyoposti ili ikiwezekana hata ukatumia mitandao hiyo kujiingizia mkwanja kuliko kutukana na watu wanaokuheshimu wakakuona hauna maana.
Usipoteze muda wako kuwajibu watu ambao hawakosi cha kuongea. Utajisumbua tu, fuata mifano ya mastaa wengi ulimwenguni, wanapoweka kitu katika mitandao ya kijamii huwa hawageuki kutazama watu wamekomenti nini baadaye.
Weka kitu chako kisha fumba macho kama huoni vile, si wote watakaokichukulia kitu chako chanya. Kuna wengine wataponda au watakutukana, ukiwajibu watu watakuona wewe mpuuzi kuliko hao waliokuanza!
Kwa leo acha niishie hapo, kuwa makini sana na mitandao ya kijamii.
0 comments: