HOFU YA EBOLA YATANDA JIJINI MWANZA: TAARIFA KAMILI HII HAPA INAYOSEMEKANA MMOJA APOTEZA UHAU
Watu sita
wakiwamo wahudumu watatu wa afya wa hospitali teule ya Wilaya ya
Sengerema mkoani Mwanza, wamewekwa chini ya uangalizi maalum baada ya
kumhudumia mgonjwa aliyefariki akiwa na dalili za ugonjwa wa ebola.Mtu
aliyefariki alitajwa kuwa ni Salome Richard (17), anayetoka katika
kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema.Akithibitisha kuwapo kwa hali hiyo
Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema, Dk. Mary
Jose, alisema mgonjwa huyo alifikishwa katika hospitali hiyo na ndugu
zake watatu akiwa na homa kali huku akitokwa na damu sehemu mbalimbali
za mwili wake.Alisema vipimo vya mgonjwa huyo vimepelekwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Tulimpokea juzi saa 7 mchana kutoka katika kijiji cha Kahunda
wilayani hapa akiwa na homa kali akitokwa damu mwilini, lakini kwa
tahadhari tulimweka wodi maalum peke yake akipatiwa matibabu na
ilipotimu saa 8 usiku alifariki dunia,” alisema
Alisema kutokana na tahadhari ya ugonjwa huo, watumishi watatu wa
idara ya afya na ndugu watatu wa marehemu huyo, wamezuiliwa kwa kuwekwa
katika uangalizi maalum hadi matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa
vitakaporejeshwa toka Muhimbili.
Akizungumzia tukio hilo, muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel
Mihayo, alisema timu maalum ya watalaam na viongozi wa mkoa walienda
hospitalini hapo juzi na kuondoka na vipimo vya mgonjwa huyo kabla
hajafariki dunia kwa kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuchukua
tahadhari linapotokea tukio kama hilo.
“Kwa sasa jamii inatakiwa kuepukana na uzushi uliozagaa kila kona
kuhusu mgonjwa huyo kufariki kwa ebola…tunawamba wasiwe na wasiwasi
kwani hatua stahiki zinachukuliwa kwa wagonjwa wa aina hiyo kama
tahadhari,” alisema Mihayo.
Mhudumu aliyempokea mgonjwa huyo katika hospitali hiyo, Fungameza
Majula, alisema ndugu watatu walimpeleka mgonjwa huyo kwa taksi lakini
alipobaini dalili hizo aliujulisha uongozi wa hospitali na mara moja
hatua za tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwazuia ndugu
kurudi nyumbani.
Hata hivyo, juhudi za kumpata mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Careen Yunusu, kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa.
Akizungumzia tukio hilo, Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw.Valentino
Bangi, alisema alipokea taarifa za mgonjwa huyo kufariki kwa homa
inayofanana na ugonjwa wa ebola au maburgh.
Bw.Bangi alisema ofisi yake imetuma timu ya wataalam wa afya katika
Hospitali ya Wilaya Sengerema na kuchukua sampuli ya vipimo vya mgonjwa
na kupeleka Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Bw.Bangi alisema ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo, tayari
taifa, uongozi wa mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na ofisi yake,
wameweka vituo vya kupima magonjwa katika mipaka ya Sirari, Mutukula na
uwanja wa Ndege wa Mwanza.
0 comments: