SAKATA LA MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI ALIYEOLEWA, MENGINE YAIBUKA
Ilikuwa Oktoba 7 mwaka huu, saa 1.00
asubuhi katika eneo la Mbondole, Kata ya Msongola, Wilaya la Ilala
mkoani Dar es Salaam kulipozuka tafrani baada ya mwanamume mmoja
kukamatwa akituhumiwa kumweka kinyumba binti mwenye umri wa miaka 15.
Mama
wa binti aliyewekwa kinyumba, Amina Juma anasema mshtuko alioupata
baada ya kumwona binti yake akichomoza katika chumba cha mwanamume huyo,
ulisababisha tumbo lake kumkata kwa uchungu.
“Sikuamini
macho yangu kumuona mwanangu akitolewa katika chumba hicho, nilitamani
iwe ndoto... lakini ilikuwa kweli na tukio hilo liliniumiza sana,”
anasema mwanamke huyo.
Akisimulia
huku machozi yakimtoka, anasema siku hiyo alipata taarifa kutoka kwa
mdogo wake kuwa mwanaye anaishi na mwanamume huyo huku akifungiwa na
kufuli ndani kwa kuhofia isijulikane.
Baada ya
kupata taarifa hizo, walishirikiana na mdogo wake kwenda kutoa taarifa
katika ofisi ya Serikali za Mtaa huo, ili waweze kumdhibiti mtuhumiwa na
kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Katika ofisi hiyo, walisaidiwa na
wajumbe wa kamati ya ulinzi ya mtaa huo, ambao walikaa kuanzia saa moja
asubuhi hadi saa 8:30 mchana ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa.
Mkasa ulivyoanza
Ilikuwa
Agosti mwaka huu mama huyo akiwa nyumbani kwake alifika kijana mmoja
ambaye alijitambulisha kuwa ni mshenga anayetaka kutoa posa kwa mwanaye.
Hata hivyo, alimkatalia na kumweleza kuwa mtoto wake bado anasoma.
“Baada ya
kumkatalia mshenga huyo akaanza kutumia mwanya wa kuja gengeni kwangu,
ili amrubuni akubali kuolewa na huyo mwanamume lakini alikuwa
anakataa,”anaelezea mama wa mtoto huyo.
Anasema
siku moja mtuhumiwa alifika nyumbani kwake na kumweleza kuwa
atahakikisha mwanafunzi huyo anafutwa shule, kwa kuwa amekwamisha mpango
wake.
“Siku
hiyo mtuhumiwa aliniongelea maneno ya ovyo, nilikasirika na kuamua
kuingia ndani kulala... nilipoamka sikumkuta binti yangu.
“Nilijaribu
kuwauliza majirani kama wamemwona, lakini sikupata jibu hivyo
nililazimika kwenda kwa mtuhumiwa ili kumwangalia,” anasema.
Alipofika
eneo hilo alimkuta kijana mmoja na kumuuliza kama mwanaye ameonekana
lakini alimjibu hakumwona, wakati huo aliiona baiskeli ya mtuhumiwa huyo
akiwa nje ikiashiria kuwa alikuwa ndani.
Anasema wakati alipokuwa anamwuliza kijana huyo, mara mtuhumiwa alitoka nje na baadaye alifuatia mwanaye.
Anasema
kitendo hicho kilimuudhi na alimua kumwadhibu kwa kumchapa fimbo ndipo
mtoto huyo alipotoroka na kwenda kwa baba yake mzazi ambaye anaishi
Kivule, Wilaya ya Ilala.
Anasema siku ya pili alilazimika kwenda kumfuata ili wafanye kikao cha ndugu kuhusiana na suala hilo.
Baada ya
kikao mtoto huyo alipoulizwa, alidai kuwa hataki tena shule.. “hivyo
nilimchukua na kwenda naye nyumbani, lakini mume wangu wa sasa (baba
mlezi wa binti huyo) alimkataa kutokana na tabia zake.”
Siku iliyofuata alilazimika kumrudisha kwa baba yake mzazi na kuwa tangu hapo hakujua tena taarifa zake mpaka lilipotokea hili.
“Mimi
naona huu ulikuwa ni mchezo uliopangwa na mtuhumiwa na baba mzazi wa
mtoto huyu, inaonekana alikuwa anajua mchezo mzima. Kama mwanaye
hakuwapo nyumbani kwa nini hakutoa taarifa polisi? Au kwa ndugu?”
anahoji.
Sakata latinga polisi
“Oktoba
10 mwaka huu nikiwa nyumbani kwangu, walikuja askari kutoka Kituo cha
Polisi Stakishari, Ukonga walichukua maelezo yangu na ya mtoto na baada
ya hapo waliniambia niende polisi baada ya siku tatu,” anasema.
Baada ya
kutoa maelezo polisi ilifunguliwa jalada la kesi ya ubakaji lenye namba
STK/RB/13749/14 na wakati huo nilipewa fomu ya polisi kwa ajili ya
kwenda Hospitali ya Amana ili vichukuliwe vipimo vyote.
“Hivi unavyoniona nampeleka mwanangu katika Hospitali ya Amana ili akapime vipimo vyote ambavyo vinahitajika,” anaeleza.
Alivyomlea mwanaye
Mama huyo
anasema aliachana na mumewe wa kwanza wakati binti huyo akiwa na umri
wa miaka miwili na kwamba tangu wakati huo, alimlea peke yake kwa hali
na mali.
Anasema
alipofikisha umri wa miaka saba, alianza darasa la kwanza na hapo
akaanza kumtembelea baba yake na hata kulala lakini hakuwahi kupewa
fedha kwa ajili ya shule.
Binti anena
Binti
huyo anasema alikutana na mwanamume huyo alipokuwa anakwenda kununua
mkaa katika banda lake lililopo katika eneo hilo la Kigezi.
Anasema mwanamume huyo alikuwa akimlaghai kwa kumwambia kuwa ameshakuwa mtu mzima hivyo aache shule aolewe.
Akiwa kwa
baba yake mzazi, binti huyo anasema mwanamume huyo alikuwa akivizia
baba huyo anapoondoka naye anamfuata na kumweleza kuwa anataka kumpeleka
mshenga, lakini baadaye alimtorosha.
“Nilianza
kuishi naye mwezi uliopita, alinitorosha kutoka Kivule kwa baba yangu
mzazi na kunipeleka nyumbani kwake Mbondole,” anasimulia.
Anasema wakati huo alimweleza kuwa ana watoto watatu wanaotakiwa kulelewa kwa kuwa aliachana na mama yao.
Mwanamume
aliyekuwa anaishi naye alikuwa anafanya biashara ya kuuza mkaa eneo la
Kigezi na kila siku alikuwa akimwachia Sh5,000 kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani.
Viongozi wa Serikali wafunguka
Mjumbe wa
Kamati ya Ulinzi wa Mtaa huo, Julius Meng’anya anasema baada ya kupewa
taarifa hizo walikwenda hadi kwenye nyumba hiyo ili kumkamata mtuhumiwa.
Walifika asubuhi eneo kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha mtuhumiwa
huyo wanamdhibiti na ilipofika saa 8.30 mchana aliporudi nyumbani kwake
walimkamata pamoja na mwanafunzi huyo.
Baada ya
kumkamata walimtaarifu mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo ambaye alifika
kwenye eneo hilo lakini cha kushangaza alimwachia huru mtuhumiwa huyo.
“Kwa
kweli kitendo cha mwenyekiti kumwachia mtuhumiwa huyo kilituudhi sana
tulitegemea mtuhumiwa angechukuliwa hatua za kisheria,” anasema
Meng’anya.
Mwenyekiti
wa Serikali ya mtaa huo, Salum Matangula alikiri kutokea kwa tukio hilo
na kusema mtuhumiwa alikiri mbele ya kikao kuwa alipewa ruhusa na mama
mzazi wa mtoto huyo ili aishi naye.
Anasema
kutokana na maelezo ya pande zote, walibaini kuwa wote wana makosa ndipo
walipomtaka mama huyo aende kwenye duka la dawa ili achukuliwe kipimo
cha mimba na baada ya hapo ampeleke mwanafunzi huyo shuleni.
“Niliwaeleza
kuwa wote wana makosa, mama alikuwa anadai mwanaye akapime kwanza,
nikamruhusu, lakini sijapata majibu hadi leo,” anasema Matangula.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Kigezi anayosoma mtoto huyo, Joseph Kalungutu
anasema mwanafunzi huyo ni mtoro na kipindi cha nyuma alikuwa
akihudhuria darasani mara moja moja na lakini kuanzia Septemba, mwaka
huu, hakuonekana kabisa shuleni.
“Mahudhurio
yake ni mabaya, baada ya kuona maudhurio yake siyo mazuri nilimwita
mama yake ambaye alidai kuwa hayupo anaishi kwa baba yake mzazi,”
anasema Kalungutu.
Anasema
Septemba mwaka huu akiwa shuleni hapo alikwenda mwanamume
aliyejitambulisha kuwa mzazi wa binti huyo akidai kuwa amekwenda hapo
kwa ajili ya kumfuta shule mwanaye kwa kuwa anaonekana mkubwa.
“Nilimkatalia
na kumweleza kuwa sheria hairuhusu mwanafunzi yeyote aliyeandikishwa
kufutwa shule hadi hapo atakapomaliza. Nilimweleza kuwa yeyote
anayejaribu kufanya hivyo lazima afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mwanamume
anayedaiwa kumtorosha binti huyo, Halifa Ally anakiri kuwa aliishi
naye... “Sina cha kukueleza zaidi ya hayo ninachofahamu huyo binti
nilikuwa naishi naye,” anasema Ally.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki anasema Ally anayetuhumiwa kuishi na
binti huyo ametoroka... “lakini polisi inawahoji mama wa mtoto huyo
pamoja na mwanaye katika Kituo cha Polisi cha Stakishari huku
tukiendelea kumtafuta mtuhumiwa ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,”
anasema Nzuki.
0 comments: