SAKATA LA ESCROW: Tunawasubiri waliochota kutoka Stanbic


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisoma ripoti yake kamati yake kuhusu kashfa ya Escrow
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisoma ripoti yake kamati yake kuhusu kashfa ya Escrow
MJADALA juu ya ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni, kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT), ungali mbichi.
Aliyetegemewa kufunga mjadala huu, kwa kushughulikia wezi halisi wa fedha hizo, ameishia kutetea uhalifu, kuhalalisha wizi, kubeba watuhumiwa na kupotosha umma juu ya waliohusika na kilichotendeka.
Akihutubia taifa juzi Jumatatu kupitia kilichoitwa, “mkutano wa rais na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” Rais Dk. Jakaya Kikwete, alikiri kuwapo udanganyifu katika kufikia utoaji wa fedha hizo.
Alikiri baadhi ya nyaraka kughushiwa. Akakiri kuwa kampuni ya Pan African Power Solution (PAP), imekwepa kodi ya serikali baada ya kulipwa fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow.
Akajitetea kuwa serikali inaitafuta kampuni ya MECHMAR iliyodaiwa kuuza asimimia 70 ya hisa zake katika kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa PAP ili iweze kulipa kodi hiyo.
Kampuni ya IPTL ni muungano wa kampuni mbili – VIP ya Rugemalira iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa na MECHMAR ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70 za hisa.
Rais alikiri kuwa aliyepewa fedha na serikali – PAP –hakuwa na sifa za kuvuna alichopata. Akakiri kuwa mmoja wa wanahisa wa IPTL, James Rugemalira, alicholipwa kilikuwa halali kwa mujibu wa sheria.
Akakiri fedha zake zililipiwa kodi ya serikali, tena kama ilivyoainishwa na mahakama.
Rais alikiri kuwa serikali yake haikufanya uchunguzi yakinifu, kuhusu historia, uhalali, sifa na uwezo wa kampuni ya PAP, katika uwekezaji wa umeme, ununuzi wa mitambo na mtaji.
Hata hivyo, pamoja na kukiri yote hayo hadharani, alishindwa kuchukua hatua dhidi ya wazembe na waliovunjaji sheria walioko serikalini.
Rais aliishia kumfuta kazi, Prof. Anna Tibaijuka, waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye kwa namna yoyote ile, hakuhusika na wizi uliotokea.
Haikutarajiwa kiongozi mkuu wa nchi kama hii, ambaye ana mamlaka makubwa ya kidola – awezaye kuvunja Bunge, kumtia mtu kizuizini, kuridhia mtu kunyongwa na kutangaza nchi kuingia vitani – kutishwa na wasiokuwa na dola.
Kitendo cha rais kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wizi huu, kimethibitisha madai ya wananchi, baadhi ya vyama vya siasa makini vya upinzani na taasisi za kiraia (NG’OS), kuwa rais “amekusudia kutenda uhalifu kwa kulinda wezi.”
Kuhusu kitendo cha ukwepaji kodi kilichofanywa na PAP, rais alikiri kuwa mamlaka ya mapato (TRA), walidai kodi kwa barua kwenda BoT.
Bali, kama PAP aliambiwa asilimlipe Rugemalira mpaka atakapolipa kodi, kwa nini hakuambiwa asimlipe MECHMAR mpaka atakapolipa kodi?Rais Kikwete amesema, Prof. Tibaijuka amepokea fedha kutoka kwa Rugamalira. Amethibitisha kuwa fedha hizo zilikuwa mchango kwa ajili ya shule ya Johanssen ya jijini Dar es Salaam.
Rais hakusema Prof. Tibaijuka hana shule. Hakusema fedha hazipelekwa shule. Hakusema fedha zilikuwa chafu. Amekiri fedha za Rugemalira zililipiwa kodi; Katibu Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Paulo Rupia, amethibitisha kupokelewa kwa fedha hizo katika shule ambayo yeye ni mlezi wake.
Rais Kikwete amesema, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow yalilipwa kwa PAP baada ya Mahakama Kuu kutoa “amri” tarehe 5 Septemba 2013. Hii siyo kweli.
Hakuna amri ya mahakama inayoelekeza fedha kutolewa. Kinachoitwa amri ya mahakama, kilikuwa ni kumaliza ugomvi wa wanahisa wa IPTL. Siyo mgogoro wa Escrow uliotokana na tozo halali ya uwekezaji na mtaji katika uwekezaji. Hiyo ndiyo amri ya mahakama.
Hakujawahi kutolewa amri nyingine yoyote ya kuruhusu fedha kutolewa katika Akaunti ya Escrow kulipwa PAP au IPTL. Wala mahakama haikuamuru kutolewa fedha hizo na serikali kama “mali iliyotekwa kwenye vita.”
Mahakama haikusema serikali ilipe fedha kutoka Akaunti ya Escrow, bila kujiridhisha na uhalali wa ununuzi wa hisa za kampuni ya IPTL, kwenda kwa PAP.
Haikuzuia serikali kuhoji kufanyika kwa malipo hayo, wakati bado kuna mgogoro kati ya serikali na Benki ya Standard Chartered (SCB) Hong Kong (BSC –HK).
Mahakama haikuagiza, wala haijaagiza serikali kutohoji, kwa nini malipo hayo yafanyike, wakati benki ya Standand Chartered, bado inaendelea kung’ang’ana mahakamani.
Benki inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow, zinastahili kuwa zake. Mpaka sasa, benki hii bado inaendelea kuhangaika mahakamani kudai haki yake.
Aidha, rais anajua kuwa mahakama haikuamuru fedha hizo kutolewa kwa PAP kwa kuwa hilo halikuwa miongoni mwa hoja zilizokuwa kwenye meza mahakamani.
Hata yeye amekiri katika hotuba yake pale aliposema, “…serikali haikuona umuhimu wa kurudi mahakamani kufanya marejeo juu ya uamuzi iliotoa.”
Hakuna shaka kama mahakama ingeelezwa vizuri kuhusu kuwapo kwa mgogoro kati ya IPTL na benki ya Standard Chartered na Tanesco na benki hiyo, isingeruhusu PAP kununua hisa za IPTL.
Amri ya mahakama iliyopo na ambayo rais amekwepa kuzungumzia, ni ile ya 17 Januari 2014.
Katika amri hii, mahakama iliamuru kampuni ya PAP kuilipa VIP Engineering Limited. Hii ni baada ya Rugemalira kushitaki karibu serikali yote mahakamani.
Rugemalira aliiambia mahakama katika hati yake ya kiapo kuwa yote yaliyofanyika, ikiwamo kutolewa kwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, ulikuwa ni “utapeli mtupu.”
Alisema, utapeli huu ulifanywa na serikali ya rais Kikwete, BoT, Benki ya Stanbic na PAP.
Kutokana na uzito wa madai ya Rugemalira, PAP na serikali zilinywea. Zikakubali kuingia katika usuluhishi wa mahakama.
Habari zinasema, suluhisho hilo halikuwafurahisha baadhi ya watu ndani ya serikali. Zikaandaliwa kampeni chafu dhidi ya Rugemalira na kampuni yake. Akaitwa mwizi.
Kazi ya kusakama wote waliopewa fedha na Rugemalira ikafanyika nchi mzima. Waliopewa mgawo, wakageuzwa wezi. Walioshiriki katika wizi, waliokwapua mabilioni ya shilingi kutoka benki ya Stanbic na waliobeba fedha kwa magunia, mifuko ya plasitiki na vikapu, wakatakatishwa.
Rais Kikwete amerejea kauli ya serikali yake bungeni, mwezi uliopita, kwamba fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow hazikuwa mali ya serikali. Amedai kuwa zilikuwa mali ya IPTL.
Amesema, ziliwekwa kwenye Akaunti ya Escrow na Tanesco badala ya kulipwa moja kwa moja kwa kampuni IPTL, kutokana na kuibuka mgogoro wa tarifu na malipo ya gharama za kuweka mtambo – Capacity Charge. Hili nalo siyo kweli. Sababu ni mbili.
Kwanza, fedha hii zilizokuwa zikisubiri kumalizika mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, haziwezi kuwa mali ya IPTL, kabla ya mgogoro kumalizika.
Katika hotuba yake hiyo, rais amekiri kuwa mpaka fedha zinatolewa, mgogoro huo ulikuwa haujamalizika. Tanesco bado inaendelea kudhulumiwa kwa kutozwa kiwango kikubwa cha malipo ya Capacity Charge.
Hakika, hotuba ya Rais Kikwete haina jipya. Imeishia kuchochea mgogoro na kuibua yale ambayo hayakufahamika.
Mathalani, Rais Kikwete amesema azimio la Bunge lililotaka serikali kutaifisha mitambo ya IPTL, halitekelezeki. Amedai kulitekeleza azimio hilo, kutasababisha kukimbiza wawekezaji nchini.
Lakini imefahamika kuwa yule ambaye rais na serikali wanaita “muwekezaji mpya katika IPTL,” hana sifa ya kuitwa mwekezaji. Huyu aweza kuitwa, “mchuuzi.”
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza Harbinder Singh Sethi, alighushi nyaraka. Siyo mwadilifu. Ni laghai na mdanganyifu.
Harbinder Singh amelipwa fedha asizostahili. Hadi anamaliza kuchota mabilioni hayo ya shilingi na akaunti ya Escrow inaamuriwa kufungwa, alikuwa hajanunua asilimia 30 ya hisa za VIP Engineering katika IPTL.
Wakati analipwa fedha hizo alikuwa hajawa mmiliki halali wa hisa katika MECHMAR.
Hii maana yake ni kwamba, wakati PAP inachotewa mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Escrow, hakuwa mmiliki halali wa IPTL.
Hadi fedha zinatolewa, alikuwa hajasajili asilimia 70 ya hisa alizodai amenunua kutoka kampuni hiyo ya Malaysia kwa Wakala wa Serikali na Kampuni (BRELA).
Kwa hali hiyo, uamuzi wa serikali wa kutaifisha mitambo ya IPTL, hauwezi kufukuza wawekezaji nchini.
Badala yake, kitendo hicho kitaongeza wawekezaji, kitarejesha heshima ya nchi na kingerudisha matumaini mapya kwa wananchi kwa serikali na chama kilichoko Ikulu.
Lakini kitendo cha kulea wezi na matapeli wengine wanaokuja kwa kofia ya “uwekezaji,” kitalifanya taifa hili kuendelea kudharauliwa.
Kuhusu azimio la Bunge lilitoka mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua dhidi ya Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Rais Kikwete amesema suala hilo ameliacha kwa mamlaka ya nidhamu.
Mamlaka ya nidhamu ambayo rais amesema amekabidhi jukumu hilo, ni Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.
Lakini uteuzi wa makatibu wakuu, haufanywi na katibu mkuu kiongozi. Unafanywa na rais. Kitendo cha rais kulikabidhi suala la Maswi kwa katibu mkuu kiongozi, ni kukwepa wajibu wake.
Naye Prof. Sospeter Muhongo, aliyetuhumiwa na Bunge kuwa dalali wa kufanikisha wizi huo, rais amedai, uchunguzi bado unaendelea. Ameeleza anayefanya kazi ya uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo, yuko nje ya nchi kikazi.
Ni muhimu Rais Kikwete akafahamu kuwa hakuna sabuni ambayo itaweza kumsafisha Prof. Muhongo katika tuhuma hizi.
Jitihada zozote za kumtetea zitaishia kudhoofisha serikali na rais binafsi.
Si hivyo tu. Sakata la wizi katika akaunti ya Escrow haliwezi kumalizika bila rais kueleza hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya maofisa wa ikulu “waliopata mgawo” kutoka kwa Rugemalira.
Sababu zilezile na makosa yaleyale ambayo rais amemtwisha Prof. Tibaijuka, anapaswa kuwatwisha pia maofisa wake wa ikulu waliolipwa na Rugemalira.
Wala sakata hili haliwezi kufungwa bila kutaja majina ya waliopokea kitita cha kati ya Sh. 800 milioni na Sh. 5 bilioni, kutoka benki ya Stanbic.
Yawezekana wakafichwa leo. Lakini hakuna mwenye ubavu wa kuficha milele na milele.
Ikiwa mkataba wa IPTL uliofungwa miaka 20 iliyopita, wakati Rais Kikwete akiwa waziri wa nishati na baadaye waziri wa fedha – bado unamtafuna mpaka sasa – hakuna awezaye kuzuai kufahamika kwa waliochota fedha Stanbic.
Watajulikana tu – kama si leo, kesho.

0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//