Washitakiwa mauaji ya Dk Mvungi wazua kizaazaa mahakamani
Sakata
hilo limetokea leo majira ya saa 4:00 asubuhi, muda mfupi baada ya
Wakili wa Serikali, Peter Njike kumueleza Hakimu Mkazi, Hellen Liwa kuwa
kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na
akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa kutajwa.
Baada
ya wakili Njike kueleza hayo, mshtakiwa Longishu Losingo alidai
mahakamani hapo kuwa Desemba 16,2014 upande wa mashtaka uliwaambia
jalada la kesi yao lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), leo (jana)
wanatuletea hadithi, tunaomba watueleze uhalisia wa kesi hii, tupo
gerezani tunateseka.
Kwa
upande wa mshtakiwa Masunga Makenza naye alidai kuwa yeye hafahamu
sheria, kesi yao ni ya muda mrefu na akahoji jalada likienda kwa DPP
linatakiwa kukaa kwa muda gani.
Makenza
alidai kuwa kesi yao ni ya kubambikiwa na kwamba ingekuwa ni kesi
halisi upande wa mashtaka ungekuwa umekwisha kamilisha upelelezi wao na
kwamba wao wapo tayari kushtakiwa ila kama upande wa mashtaka umeshindwa
kukamilisha upelelezi mahakama iwaachie huru, wakikamilisha
watawakamata tena.
Wakili
wa Serikali, aliieleza mahakama kuwa wameyasikia malalamiko hayo na
kwamba yote yanajikita katika kuchelewa kukamilika kwa upelelezi na
kwamba watahimiza na kufuatilia upelelezi ukamilike mapema.
Jibu
hilo halikuwaridhisha washtakiwa hao, mshtakiwa Longishu alisema
“Tumechoka kwa kweli tumechoka hatuna ugomvi na mahakama wala magereza
ila tunaugomvi na waendesha mashtaka kama wameshindwa kukamilisha
upelelezi watupeleke polisi.”
Yote
kwa yote washtakiwa hao, wakaiambia mahakama kuwa kutokana na hoja hizo
za upande wa mashtaka leo (jana) hawapo tayari kushuka kizimbani,
watakaa chini hadi waelezwe jalada leo lipo wapi na kesi imefikia katika
hatua gani.
Baada
ya washtakiwa hao wote kugoma kushuka kizimbani na kukaa chini
wakisubiri kuelezwa hatma ya kesi yao, Hakimu Liwa aliwasihi wakubali
kuondoka kizimbani hapo kwa sababu yeye siyo hakimu husika ameitaja tu
kesi yao, wamsubiri hakimu husika, Waliarwande Lema wamueleze malalamiko
yao.
Maelezo
hayo ya hakimu Liwa walikubaliana nayo na kwa pamoja wakainuka na
kuelekea mahabusu ya mahakama kwa ajili ya kupelekwa mahabusu na kesi
iliahirisha hadi Januari 13,2015.
Washtakiwa
wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi (32), John
Mayunga (56),Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40),
Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya (30), Ahmad Kitabu (30).
Kwa
pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la
mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya
16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
0 comments: