HAYA NDIO MAOVU YANAYOFANYIKA GEREZANI..HII NI RIPOTI MAALUM YA UKWELI NA TUNAOMBA HAYA MAMBO YASHUGHULIKIWE NA WAHUSIKA




WIKI iliyopita mfungwa aliyemaliza kifungo chake alieleza kwa kina jinsi alivyoingiza simu na bangi gerezani na kuzitumia kama mradi wake wa kujipatia pesa. Pia watu wengine wawili waliowahi kufungwa katika magereza ya Segerea, Mwanga na Karanga mkoani Kilimanjaro nao wameeleza jinsi walivyokuwa wakitoa pesa kupewa chakula kizuri gerezani.

Biashara ya chakula
Mmoja wa watu hao alisema: “Ukitaka kupata chakula kizuri katika Gereza la Segerea ilikuwa lazima ununue kutoka kwa wapishi.

“Unachoweza kukifanya ni kuzungumza nao halafu unawalipa kwa wiki. Chakula ambacho unaweza kukipata ukiingia mkataba huo ni mboga iliyoungwa kwa mafuta na ugali”.

Anasema kama huna cha kuwapa kwa wiki hiyo unaweza kuwasiliana na ndugu yako akampa fedha mmoja wa askari magereza wanaopeleka mahabusu mahakamani akaziingiza magereza.

Mtu mwingine ambaye ameonja kifungo katika gereza la Karanga na Mwanga mkoani Kilimanjaro alisema; “Rushwa ndani ya magereza ni kubwa kiasi kwamba, ukiwa huna pesa ya kuhonga askari, mnyapara au daktari wa magereza, utakiona kifungo kibaya mno”.

Akisimulia jinsi alivyoingiza simu magereza, Mfungwa huyo ambaye alitumikia kifungo cha miaka minne katika magereza mkoani Kilimanjaro, alisema aliingiza simu gerezani baada ya kushuhudia askari mmoja wa magereza akimpiga mfungwa ambaye baadaye alifariki dunia.

Kutokana na tukio hilo, askari huyo baada ya kuambiwa na baadhi ya wafungwa kuwa aliyeshuhudia tukio hilo ana uwezo wa kuvujisha taarifa hiyo kwa watu wengine nje ya gereza aliamua kujenga naye urafiki.

Anasema askari hiyo alimwahidi kuwa atamsaidia kuingiza simu gerezani ambayo aliitumia muda wote kuwasiliana na mke wake na marafiki zake.

Alisema, "Simu hiyo ilinisaidia kupata habari za kila siku za familia yangu na pia niliwapigia watu mbalimbali bila matatizo,"

Mfungwa huyo, anasema uhalifu unaofanywa na askari magereza ndio unaosababisha kutoa mwanya kwa wafungwa wa kiume kujiingiza katika vitendo vya kuvunja sheria, ikiwamo kuingiza bangi, simu na kufanya mapenzi na wanawake wa nje ya gereza.

Anasema wakati mwingine askari magereza wanashirikiana na wafungwa kuiba mali za gereza, ikiwamo mahindi na mbolea na kuuza uraiani.

Anatoa mfano kuwa, kuna siku alishirikishwa na askari mmoja katika Gereza la Karanga kuiba magunia saba ya mahindi.Alifahamisha kuwa waliyapakia katika lori kwenda kupanda shamba la gereza, lakini badala yake waliyauza kwa watu waliokubaliana na askari huyo.

Alidai kuwa baada ya kuuza alipata mgawo wake pamoja na wafungwa wenzake wanne waliokuwamo ndani ya gari hilo.

Mbali ya kushirikishwa katika wizi huo wa mahindi ya magereza, pia alidai kuwa wahi kutumiwa na askari huyo kuiba mbolea ya ruzuku ambazo zinatolewa na serikali kwa gereza hilo.

Vilevile, kwa kushirikiana na baadhi ya askari magereza alisema aliwahi kuingiza vitu mbalimbali gerezani ikiwamo pesa na bangi kwa ajili ya kuiuza.


Kuhusu kufanya mapenzi na wanawake nje ya magereza, alisema hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Anasema wafungwa wengi wenye uwezo huwapa pesa askari wasiokuwa na maadili hivyo kupangiwa kufanya kazi nje ya gereza.

Alisema: "Unachotakiwa kufanya ni kupanga na askari magereza ambaye anampa taarifa mke wako kuwa mtakuwa wapi."

Mfungwa huyo anasema: Akifika mke wako, askari magereza anakuruhusu kwenda sehemu yoyote ya kificho karibu na eneo hilo.Alifahamisha njia nyingine ambayo inaweza kukufanya ukutane na mke wako ni kwenda kulazwa hospitalini.

“Asilimia kubwa ya wafungwa wanaolazwa hospitali huwa sio wagonjwa, bali hupata kibali cha kwenda kutibiwa baada ya kutoa chochote kwa daktari wa gereza,” alifahamisha na kuongeza."Usione ndugu yangu wafungwa wengi wamelazwa hospitalini, wengine wanakuwa sio wagonjwa, wapo huko kupumzika na kupata nafasi ya kuonana na ndugu zao kirahisi,"

Alieleza kuwa: “Ukipata kibali cha kwenda kutibiwa hospitali, unaweza kumpa chochote askari anayekulinda akakuruhusu kukutana na mkeo usiku.

Vilevile, sehemu nyingine ambayo mfungwa anaweza kuitumia kukutana na mke wake ni pale anapopangiwa kufanya kazi kwenye mashamba ya maafisa wa magereza ambako hupata uhuru zaidi.

"Mfungwa kufanya kazi kwenye mashamba ya maafisa wa magereza ni kosa ndiyo maana wanapokuchukua huwa wanatoa uhuru kiasi, hasa kwa wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo, au wenye tabia njema," alifahamisha.

Hata hivyo alisema, ingawa kuna wafungwa ambao wapo hospitali kwa ajili ya kuishi vyema, wapo wafungwa ambao wanaumwa ambao wanahitaji kupatiwa matibabu, lakini hawapelekwi hospitalini.

Alidai kuwa kuna usanii mwingi katika magereza, kwani hata Tume ya Haki za Binadamu wanapopita kuangalia hali za wafungwa baadhi ya viongozi wa magereza hutandika mashuka mapya katika magodoro ya wafungwa, lakini wakiondoka tu huyaondoa haraka.

Ripoti ya Tume
Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka 2 imeonyesha kuwa chakula kikuu katika magereza nchini ni ugali na maharage. Mboga za majani, nyama, wali na matunda huliwa baadhi ya siku katika wiki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ilibainika kuwa asimilia 59.2 ya wafungwa waliohojiwa walikiri kuwa chakula kinatosha kama kitasimamiwa na kuboreshwa huku asilimia 40 walikiri kuwa chakula hakitoshi.

Tume inapendekeza kuondolewa kwa matumizi ya mitondoo magerezani kwani hali hii imejitokeza zaidi katika mabweni ya wafungwa wa kunyongwa mfano gereza la Isanga, Ukonga, Uyui na Gereza la Mahabusu la Morogoro.

Tume inashauri upekuzi wa wafungwa kwa kuwavua nguo hadharani utafutiwe njia mbadala kwa vile utaratibu wa sasa unavunja haki ya faragha na staha ya mtu.

Aidha, kuna fursa ya kutembelewa na ndugu zao na kuonana nao ana kwa ana. Magereza yote yametayarisha sehemu maalumu na taratibu za kufuatwa wakati wafungwa na mahabusu wanapowasiliana na jamaa zao.

Msemaji Magereza
Hata hivyo, wiki iliyopita Msemaji wa Jeshi la Magereza, Mtiga Omari alisema kuwa jeshi lake limekuwa likipambana na vitendo hivyo viovu na kwamba wapo watu wengi wakiwamo raia na wafungwa ambao wamefunguliwa kesi za kuwasaidia wafungwa kumiliki simu gerezani.

Mtiga alisema jeshi hilo lina mambo mengi ambayo wananchi wanapaswa kuyajua, lakini atayazungumzia kwa ruksa ya Kamishina wa Magereza, Augustine Nanyaro.
chanzo:bossngassa

0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//