Kafulila: watimueni kabla ya Bunge
Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila amesema kuna kila
sababu wahusika wote wa sakata la uchotwaji Sh306 bilioni kutoka Akaunti
ya Tegeta Escrow, wawe wamefukuzwa kazi kabla ya kuanza kwa mkutano
ujao wa 18 wa Bunge.
Pia, amesema fedha zilizochotwa zirejeshwe kama ilivyokuwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na wafikishwe mahakamani.
Akihutubia
mamia ya wananchi kwenye Viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam
jana, Kafulila alisema kilichojitokeza katika ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya ufisadi huo ni ‘trela’ na
picha kamili iko katika ripoti ya Takukuru.
“Tunataka kabla ya mkutano kuanza wahusika wote wafukuzwe kazi kwani wamesababisha hasara isiyohitaji mjadala.
“Kama
ambavyo fedha za Epa zilirejeshwa, na fedha za Escrow nazo zinatakiwa
kurejeshwa na zielekezwe katika miradi mingine ya maendeleo kuliko
kuwafumbia macho hawa,” alisema Kafulila.
Hadi
sasa, Rais Jakaya Kikwete ameshamfukuza kazi Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka huku akimweka ‘kiporo’
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine
waliofikwa na kadhia hiyo ni katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kupisha uchunguzi, huku aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema akijiuzulu wadhifa wake
kwa maelezo kuwa ushauri wake haukueleweka.
Kafulika
alisema: “Kuna ripoti ya PCCB ambayo imefichwa na serikali kuhusu
sakata hili la escrow na hii tunayoipigia kelele ni trela kwani hiyo ya
PCCB ndiyo ina majina na kiasi cha fedha walichokuwa.”
0 comments: