CCM kutumia panga la 2005, IJUE HII KWA KUISOMAA HAPAA
Vigezo 13 vilivyowekwa na CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa 2005 kumpima mwanachama anayefaa kugombea urais, ndivyo
vitakavyotumika kuwaengua makada wanaoendelea kujitokeza kuwania nafasi
hiyo mwakani, imefahamika.
Vigezo hivyo vinaonekana kuwa kizingiti
kwa baadhi ya makada wa chama hicho ambao tayari wametangaza na wengine
wanaotajwa kutaka nafasi hiyo ya juu nchini, ukiachilia mbali mnyukano
unaotarajiwa kutoka vyama vya upinzani vinavyoonekana kupata nguvu.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip
Mangula amelithibitishia gazeti hili kwamba, “Sifa hizo 13 zilizotumika
mwaka 2005 na 2010 ndizo zitakazotumika pia mwaka 2015 na wala
hakutakuwa na maboresho wala nyongeza ya aina yoyote.”
Vigezo hivyo viliwekwa ili kuhakikisha
chama hicho kinampata mgombea asiyetiliwa shaka juu ya vitendo vya
uadilifu, mwenye uzoefu wa uongozi serikalini, atakayedumisha muungano,
mwenye upeo wa masuala ya kimataifa, mtetezi wa wanyonge,
asiyejilimbikizia mali na mwajibikaji, mambo ambayo hata hivyo, bado
yameibua mjadala iwapo yanazingatiwa au la.
Pia anayetakiwa lazima awe mwenye
kuzitetea sera za CCM, anayekubalika na wananchi, asiye na hulka ya
udikteta au ufashisti, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara na
kiwango cha elimu ya chuo kikuu au inayolingana nayo.
Licha ya vigezo hivyo, baadhi ya makada
waliokwishajitokeza na wengine wanaotajwa wanaonekana dhahiri kukosa
baadhi sifa hizo na wengine wako ‘kifungoni’ kwa miezi 12 baada ya
kupewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo
vinavyokiuka maadili ndani ya chama na jamii.
Vigogo wa CCM ambao wanatajwa kutaka
kupewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho ambao iwapo
watachukua fomu, watatazamwa kwa vigezo hivyo ni Mbunge wa Nzega, Dk
Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba ambao wamekwishatangaza kuwania nafasi hiyo.
Wengine ambao wanatajwa ingawa
hawajatangaza nia hadharani ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa;
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa; Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu); Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wachambuzi wanavyosema
Akizungumzia vigezo hivyo, Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Tumaini, Danford Kitwana alisema CCM inajua kuwa hakuna
mgombea anayeweza kuwa na sifa zote 13, kwa hiyo inapaswa iangalie ni
nani anawazidi wengine.
“Kigezo cha kuwa na sifa ya maadili
ndicho kinachowakwamisha wengi, pia hakuna mgombea anayeweza kuwa na
sifa zote zilizowekwa na chama, mwingine anaweza kuwa na sifa saba, nne
au tano.
“Wakitumia mfumo wa kuwatazama wagombea wao kwa idadi ya sifa, mtu mwenye sifa nyingi ndiye asimamishwe kugombea.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania
(OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema Tanzania inahitaji kuongozwa na rais
mwenye historia ya uadilifu wa matumizi ya fedha za umma.
“Tunahitaji kiongozi anayeweza kusimamia
fedha za umma, si mtu anayenunua vitu ovyo bila kujali Hazina kuna
kiasi gani, hilo ni tatizo kubwa,” alisema Dk Mallya.
Aliongeza kuwa, kiongozi huyo lazima awe
mchapakazi anayeweza kuwaletea wananchi maendeleo, lakini watu wengi
wamekuwa wakisema wanamtaka mtu mwadilifu bila kuzungumzia uwezo wake wa
kufanya kazi.
Mwalimu mstaafu wa shule ya msingi,
Rehema Mathayo alisema kutokana na baadhi ya viongozi ndani ya CCM
kukumbwa na kashfa za ufisadi, anayetaka kugombea urais lazima awe
‘msafi’ ndani na nje ya chama.
“Mshindi ndani ya chama ni mtu
atakayekuwa amewashinda wenzake kwa kuwa na maadili mazuri na asiwe na
doa lolote la kujishughulisha na ‘dili’ za ajabu,” alisema Rehema.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa mgombea huyo
lazima awe na uzoefu mkubwa wa masuala la kimataifa kwa kuwa hata kama
atakuwa na maadili, kama hafahamu namna ya kuwaunganisha wananchi na
jumuiya za kimataifa, hatakuwa na manufaa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Ernest Mwasalwiba alisema kutokana na kuporomoka kwa maadili hususan kwa
viongozi wa umma, vitendo vya rushwa na kadhia mbalimbali, rais ajaye
anatakiwa kuhakikisha yale anayoyasema ndiyo anayatenda na Watanzania
hawahitaji Rais dikteta.
“Masuala ya maadili, rushwa, yote haya
yanazuiwa mpaka sasa lakini suala ni usimamizi tu... ni wakati sasa wa
rais ajaye kuonyesha ajenda yake itakuwa ipi, anapokuwa amesema kitu
kila mtu lazima afuate mfano akisema anachukia rushwa na maadili kwa
yaheshimiwe isiwe ni mjadala kila mtu anafuata kuanzia chini hadi juu.
“Dikteta siyo kiongozi tunayemtaka, bali
tunataka kiongozi atakayesimamia sheria na mifumo iliyopo iweze kufanya
kazi ipasavyo... mfano Rais Jakaya Kikwete kipindi anaingia aliingia na
kaulimbiu ya ‘Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya’ ambayo ilifuatwa hadi
na viongozi wa halmashauri.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Romanus Dimoso alisema: “Sifa za rais huwa zinajulikana. Tunahitaji rais
ajaye anayejua hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa, hatutaki rais ambaye
hatambui mchango unaotolewa na vyama vingi vya siasa na jinsi
atakavyoweza kufanya navyo kazi hususan kwa kuhakikisha demokrasia
inazingatiwa.”
Aliongeza: “Je, malengo ya anayetaka
urais yale ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi hii inafikia uchumi wa
kati. Amejipanga vipi kama mtumishi wa kwanza wa Taifa hili kutufikisha
huko?... Hatutaki mtu awe rais tu kwa jina.”
Rais mstaafu wa Chama cha Madaktari
Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema: “Tunahitaji rais anayeweza
kufanya uamuzi mgumu kwa mustakabali wa Taifa, asiwe rais wa maneno
maneno, bali wa vitendo. Anasema dawa hospitalini hakuna na kesho
zinakuwapo.
“Tunataka mtu mwenye historia ya
uongozi, ameshawahi kufanya nini katika kuboresha sekta ya afya, elimu,
uchumi na kijamii? Alishafanya maamuzi magumu yapi ambayo kila mmoja
aliyaona na aliyaheshimu?”
Imeandaliwa na gazeti la Mwananchi
0 comments: