MVUA ILIYONYESHA KWA MASAA MAWILI TU YAANIKA UDHAIFU MKUBWA WA JIJI LA DAR ES SALAAM.

Magari yakipita katika makutano ya barabara za Morogoro na bibi titi Dar es Salaam baada ya mvua iliyonyesha kwa saa mbili jana.


Dar es Salaam.
Mvua iliyonyesha kwa saa mbili katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jana, imeleta kero kwa wasafiri wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu na kusababisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika kutokana na kujaa maji.


Mvua hiyo iliyoanza saa nne asubuhi hadi saa sita mchana, ilisababisha baadhi ya barabara kutopitika ikiwamo ile ya Samora karibu na Jengo la Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya maeneo ya Upanga na Msasani.


Aidha, watumiaji wa Barabara za Azikiwe, Bibi Titi na Morogoro katikati ya jiji walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji hayo ambayo yalionekana kuchanganyika na majitaka yaliyotokana na baadhi ya chemba kujaa.


Eneo linalojengwa njia za mabasi ya haraka katika eneo la Akiba, lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo vya moto na watembea kwa miguu.


Maeneo ya Kariakoo, Barabara ya Uhuru na Msimbazi, yalijaa maji kama ilivyokuwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuelekea Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo zilikuwa hazipitiki kutokana na mvua hizo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.


Wakazi wa mabondeni walianza kuingiwa na hofu ya kukumbwa na mafuriko wakati hali ya hewa ilipokuwa inabadilika huku mvua ikiongezeka kwa kasi. Katika bonde la Msimbazi, Kigogo na Jangwani wakazi walionekana wenye hofu baada ya mvua kuongezeka.


Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alikataa kusema lolote na kusukuma mpira kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgurumi.


Hata hivyo, Mgurumi alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Agnes Kijazi alisema hayo ni matokeo ya taarifa ya hali ya hewa waliyoitoa Oktoba, Novemba na Desemba ambayo yalibainisha kuwa kutakuwa na vipindi virefu vya jua katika msimu wa mvua pamoja na mvua kubwa. Alisema mvua zilizonyesha jana, zinanyesha mwisho wa msimu wa mvua kama ilivyotabiriwa kabla.


Kijazi alisema kesho (leo) wanatarajia pia mvua kubwa kutokana na kuwapo kwa mkandamizo mkubwa wa hewa katika pwani ya Madagascar.


“Kesho (leo) tutatoa taarifa nyingine ya hali ya hewa kwa kipindi cha miezi mitatu mingine, hivyo wananchi watumie taarifa hiyo katika mipango yao mbalimbali,” alisema mkurugenzi huyo.


Wakazi walonga
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, wakazi wa mitaa hiyo walisema hali hiyo ya chemba kufurika imeshakuwa sugu na hakuna mikakati thabiti wa kukabiliana na tatizo linapotokea.


Dereva taksi katika Mtaa wa Azikiwe, Frank Emmanuel alisema jiji linatoa harufu ya majitaka, hususan kuanzia Jengo la Benjamin Mkapa hadi kituo cha mafuta katika makutano ya barabara za Upanga na Azikiwe. “Eti ndiyo wanasema mjini hapa! Mvua imenyesha kidogo maji haya ya kinyesi yamejaa na kuleta adha kwa wananachi… hii ni hatari kwa afya zetu.”


Mkazi mwingine, Mustafa Said alizitupia lawama mamlaka husika kwa kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo akisema hali hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara wakati wa mvua.


“Mvua hii ikiacha kunyesha na wakishaona na kusoma katika vyombo vya habari kesho watakuja kufanya matengenezo lakini baada ya muda mfupi mambo ni yaleyale,” alisema Said.


Mkazi mwingine, Josephine Joseph aliitaka Manispaa ya Ilala kulishughulikia suala hilo ambalo alisema limekuwa kero hususan maeneo ya Akiba katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi Titi kwani mara kwa mara mvua inaponyesha maji hujaa.


“Wakati mvua ikiendelea kunyesha hapa magari hayawezi kupita, maji haya yenye kinyesi yalijaa hadi kule upande wa pili. Tunaiomba manispaa ishughulikie kero hii,” alisema akiwa katika kituo cha CBE akisubiri usafiri kwenda Mwananyamala.


Alichowahi kusema RC
Desemba 16, mwaka huu wakati akifungua kikao cha kwanza cha wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Said Mecky Sadiki aliwataka wahandisi wanaosimamia ujenzi wa miradi ya barabara katika jiji hilo kuhakikisha wanawasimamia ipasavyo makandarasi wanaojenga miradi hiyo ili ikamilike kwa viwango na muda uliopangwa na kuwaondolea wananchi adha ya usafiri na barabara kujaa maji nyakati za mvua.


Katika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam, zaidi ya Sh88 bilioni zilipendekezwa kuidhinishwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa lengo la kufanya ukarabati wa kawaida, matengenezo ya barabara za zamani na mpya kwa kiwango cha lami na ujenzi wa madaraja mapya na yale yaliyoharibiwa wakati wa msimu uliopita wa mvua.


Alizitaka mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam, kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaovunja sheria kwa kujenga majengo na kuta katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuziba mifereji ya maji na kubomoa kingo za mito hali inayosababisha mafuriko katika makazi ya watu wakati wa msimu wa mvua.MWANANCHI

0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//