Maiti ya mwanamke iliyofukuliwa Shinyanga yazikwa kwa mara ya pili

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na wananchi wa Mtaa wa Masekelo, Manispaa ya Shinyanga wamelifukia kaburi la Benadetha Steven (35) aliyezikwa na kifaranga tumboni lililofukuliwa juzi na watu wasiojulikana kwa madai ya imani za kishirikina.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Shinyanga, Musa Talib jana alilaani kitendo cha kufukua kaburi hilo la Benadetha aliyefariki dunia Januari 3 mwaka huu.
Taibu alisema tukio hilo halivumiliki, hivyo aliwataka wananchi kushirikiana na polisi kufanya uchunguzi.
Alisema wao pekee hawawezi kujua kinachofanyika, huku akiweka wazi kuwa kaburi hilo halijatitia bali kuna watu wanaofanya mambo ya kishirikina.
“Mtu mwenye dini hawezi kufanya hivyo hizi ni imani za kishirikina haya mambo ndiyo yanafanya watu waende kwa waganga wa kienyeji, hebu tujiulize mtu ameshafariki dunia na kuzikwa, unakwenda kufukua kaburi lake unatafuta nini? Tushirikiane kuwabaini waliofanya kitendo hiki,” alisema Taibu.
Taarifa za kufukuliwa kaburi hilo zilianza kusambaa juzi saa 1.00 usiku.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Kata ya Masekelo, Josephina Kishiwa alisema alipata taarifa za tukio hilo juzi.
“Hili ni tukio la mara ya kwanza kutokea katika makaburi haya, hatujawahi kukuta kaburi limefukuliwa...kwa kweli hiki kitendo kimetusikitisha sana, tunaomba tu Serikali ifanye uchunguzi ili tujue chanzo cha tukio hil,” alisema Kishiwa. Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mapinduzi Kata ya Ndala, Deo Masanja alisema hawaamini kama fisi wanaweza kufukua kaburi hilo.
Alisema wakati wanamzika marehemu walichimba kaburi refu, lakini leo wanashangaa kuona limekuwa fupi hadi jeneza na sanda vinaonekana.

0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//