DARASA LA MAHABA :Wajua Jinsi ya Kumdhibiti Mpenzi Anayepiga Mizinga?


Baada ya hayo sasa tunarudi katika mada yetu ya leo, nazungumzia juu ya tabia za baadhi ya watu walio katika uhusiano kupenda kuwapiga 'mizinga' sana wenzi wao. Tabia hii ipo zaidi kwa upande wa wanawake, ingawa siku hizi hata wanaume nao wameingia katika mkumbo huu.

Siyo ajabu kumsikia mwingine akisema; "Mimi nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nitakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri, maisha yanaendelea. Yaani ni full kujiachia."

Si hivyo tu, wapo wanaume ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.

Unaweza kumsikia mwanaume akisema; "Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananinpa anajua akinizingua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia. Yule ndiyo mwanamke wa kuwa naye bwana!"

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze kwamba huna kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana katika kutatua tatizo linalomkabili.

Itakuwa sio busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili. 

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ?out?, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au hana. Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka?

Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu nani? Fanya mabadiliko tafadhali. Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo sio ya msingi, vipengele vifuatavyo vinafaa sana kwako...

MWELEZE UKWELI
Kama huna pesa wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile. Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana pesa au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ?mizinga? ili afaidi.

Ishi kawaida, kuwa mkweli kwake siku zote, utakapokuwa mkweli kwake atakuheshimu kwa uwazi wako. Siku zote zilingane, uwe una fedha au huna asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa sana katika maisha yako ya kimapenzi.

JENGA MAZINGIRA YA YEYE KUKUSAIDIA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

BANA MATUMIZI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli ulionao moyoni ni kwamba huna fedha za kutosha. 

Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakusababishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga 'mizinga' mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo. 

NAWAPENDA SANA!!!

0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//