Kamati ya Bunge yataka Ofisa Utumishi Nkasi ashushwe cheo

Mwenyekiti wa kamati ndogo ya bunge ya hesabu za serikali Ferister Bura

KAMATI ndogo ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeitaka Wizara inayohusika na Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Tamisemi) kumuondoa na kumshusha cheo Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Nkasi, Deogratias Mboya.
Wametaka hatua hiyo ichukuliwe dhidi yake kutokana na uzembe alioufanya katika ofisi yake uliosababisha wakuu wa idara zote za halmashauri hiyo kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu sasa.
Pia halmashauri hiyo imeagizwa kushirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuhakikisha inajibu maagizo manne na hoja 21 za ukaguzi haraka iwezekanavyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo , Felister Bura ambaye pia aliongeza kuwa ofisa huyo amekuwa sababu ya idadi kubwa ya watumishi wa halmashauri hiyo kutopandishwa vyeo na kuwa na wakuu wengi wa idara wanaokaimu.
“Wakuu wengi wa idara katika halmashauri hii wanakaimu wengine zaidi ya miaka sita na nane tena wenye sifa stahiki hii ni dhambi; ashushwe cheo ili naye aone maumivu yake huu ni uzembe wa hali ya juu hatuwezi kuuvumilia,“ alisisitiza.
Kaimu mwanasheria wa halmashauri hiyo, Gabriel Lunyamila aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu amekuwa akikaimu nafasi hiyo licha ya kuwa na sifa stahiki.
“Nilianza kama Ofisa kata 1993 na baadae nikajiendeleza na kuwa mwanasheria katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kisha mwezi Machi 2011 nikahamishiwa katika halmashauri hii ya Nkasi hadi kufikia Oktoba mwaka jana nadai zaidi ya Sh milioni moja ikiwa stahiki zangu za kukaimu nafasi hii ambazo bado sijalipwa,“ alieleza.
Kwa upande wake, Ofisa Usimamizi Fedha wa Tamisemi na Mratibu wa Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa Wizarani, Fauzia Hamidu alikiri kuwa tatizo kubwa katika halmashauri ya Nkasi ni kutopandishwa vyeo kwa watumishi wake na pia idadi kubwa ya wakuu wa idara wanakaimu.
Alisema tatizo lipo kwa Ofisa Utumishi ambaye amechelewesha kuwasilisha mchakato wa kupeleka katika vikao husika kufanyiwa kazi.


0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//