Kampuni 3 zataka jengo la ATCL lipigwe mnada

Jengo la ATCL

KAMPUNI tatu zimewasilisha ombi la kupigwa mnada kwa jengo la Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufidia deni la dola za Marekani 1,182,595 ambazo zinadai shirika hilo.
Kampuni zilizowasilisha ombi hilo katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara ni Kampuni ya huduma za utalii ya Leisure Tours and Holidays, Wellworth Hotels & Lodges Ltd na kampuni ya Pembejeo ya Tanzania Bags Corporation (1998) Limited (TBC).
Deni hilo linatokana na kesi mbalimbali zilizofunguliwa na kampuni hizo. Leisure Tours and Holidays inadai ATCL dola za Marekani 477, 506.38, Wellworth Hotels & Lodges Ltd inadai dola 661,089 na TBC inadai dola 44,000.
Januari 8 mwaka huu, kampuni hizo kupitia Wakili wao, Jerome Msemwa ziliandika barua kwa Msajili wa Mahakama ya Biashara, zikiomba mahakama iendelee na utekelezaji wa tuzo kwa kuamuru jengo la ATCL lililopo katika Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, liuzwe kufidia madeni yao.
Kwa mujibu wa barua hiyo, kulikuwa na makubaliano ya utekelezaji wa hukumu ya mahakama, yaliyofanyika mahakamani Septemba 17, mwaka jana.
ATCL ilitakiwa kulipa madeni hadi kufikia au kabla ya Desemba 31, mwaka jana, lakini imeshindwa kufanya hivyo hadi sasa.
Kupitia barua hiyo, wadai hao wanaomba mahakama iteue dalali kwa ajili ya kuuza jengo hilo, kufidia kiasi wanachodai, bila kuchelewa.
Awali katika makubaliano yao, ATCL na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, ziliahidi kulipa madeni hayo yote kwa awamu tatu; Kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana, lakini hadi sasa kampuni husika hazijalipwa.
Jengo la ATCL lilishafanyiwa uthamini, kutokana na amri ya Mahakama iliyotolewa Februari 11, mwaka juzi na kubainika kuwa lina thamani ya Sh bilioni 12.
Amri ya uthamini wa jengo hilo, ilitolewa katika kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Leisure, ambayo pia iliwasilisha ombi la kuuzwa kwa jengo hilo kufidia deni lake, baada ya ATCL kushindwa kutekeleza makubaliano waliyofikia nje ya mahakama katika kesi ya madai Namba 56 ya mwaka 2009.
Kampuni hiyo ilikuwa ikidai ATCL dola 716,259.25 baada ya kushindwa kulipia huduma za ukodishaji wa magari.


0 comments:

Copyright © 2013. MAPYATZBLOG - All Rights Reserved
Customized by: MAPYATZBLOG | Powered by: http://bongoswagzs.blogspot.com/
Designed by: http://bongoswagzs.blogspot.com//